KAMATI ya uchaguzi ya chama cha soka mkoa wa Arusha (ARFA) imeweka hadharani majina ya wagombea waliopita katika usaili uliofanyika Desemba 10 mwaka huu chini ya usimamizi wa mjumbe wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Wagombea waliopita kwenye usaili huo na nafasi wanazowania kwenye mabano ni Omary Walii na Peter Temu (Mwenyekiti), Zakayo Mjema (Katibu Mkuu), Mwarizo Nasorro (Katibu mkuu msaidizi), Omary Nyambuka (Mweka Hazina).
Wengine ni Athumani Mhando, Hamiss Issa (mjumbe mkutano mkuu TFF), Soud Maohamed (mjumbe kamati ya Utendaji ya ARFA).
Walioenguliwa baada ya kushindwa usaili ni James Rugangila, Fredrick Lyimo, Gerald Munisi, Maiki Warioba na Victor Mwigila.
Katibu wa kamati ya uchaguzi ya ARFA, Selemani Kilua alisema baadhi ya wagombea hawakukidhi vigezo na sifa ambazo miongoni mwa vigezo hivyo ni cheti cha kidato cha nne na uzoefu wa miaka mitano katika uongozi.
“Tuliwatangazia wagombea wote kuwa siku ya usaili lazima waje na cheti halisi cha elimu ya kidato cha nne na si nakala na kwa kulizingatia hilo ndiyo maana mgombea ambaye hakuja na cheti halisi naye alienguliwa ili uchaguzi uwe wa haki,”alisema Kilua.
Awali wagombea 13 walijitokeza kuwania nafasi mbali mbali ambazo ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina, Mjumbe wa Mkutano Mkuu, Mjumbe Mwakilishi wa klabu na wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji. Uchaguzi wa ARFA umepangwa kufanyika Januari 8 mwakani.
ConversionConversion EmoticonEmoticon