ELIBARIKI Kingu, Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi anatuhumiwa kuchochea kuongezeka kwa vitendo vya uvamizi katika msitu wa hifadhi wa Minyughe, wilayani Ikungi, anaandika Mwandishi wetu.
Mbunge huyo anadaiwa kuwalipia faini wananchi ambao wamekuwa wakikamatwa, kushtakiwa na kuhukumiwa mahakamani kwa makosa ya uvamizi wa msitu huo. Anadaiwa kutumia nafasi hiyo kama jukwaa la kisiasa la kumuongezea ushawishi kwa wananchi.
Taarifa hizi zinakuja wakati ripoti zikiwa zinaonesha kuwa zaidi ya wakazi 41 wa kijiji cha Mtavira, kata ya Makilawa, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida wamefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Ikungi kwa tuhuma za kuvamia msitu wa hifadhi ya Minyughe.
Michael Lyimo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) amesema, “Tuafanya juhudi kubwa lakini bado matokeo siyo mazuri sana kwani wananchi waliohukumiwa kwa uvamizi wanalipiwa adhabu ya faini na Mbunge wao. Kama wangelipa wenyewe wangeona umuhimu wa kutovamia msitu wa hifadhi.”
Lyimo amedai kuwa wanasiasa wamekuwa wakiutumia msitu huo kujipatia umaarufu wa kisiasa na kusaka kura kwa kuwashawishi wananchi kuwa waendelee kuishi ndani ya msitu huku wanasiasa wengine wakiahidi kuufanya msitu huo wa hifadhi kuwa eneo la makazi iwapo watachaguliwa.
Mpaka sasa, jumla ya kaya 76 zilizokuwa zikiishi katika nyumba zilizokuwa ndani ya hifadhi zimehamishwa kwa nguvu na nyumba hizo kuvunjwa.
“Nawasihi wanasiasa watafute namna nyingine ya kuomba kura na kutafuta umaarufu wa kisiasa kwasababu uhifadhi wa mazingira una faida nyingi hata kwa kizazi kijacho, hivyo historia itakuja kuwahukumu waharibifu wa mazingira,” amefafanua Lyimo.
ConversionConversion EmoticonEmoticon