Propellerads

Mawakala wa mbegu wenye mbegu feki kufutiwa usajili



Image result for picha za pamba

HIVI karibuni nilipata fursa ya kuzungumza na Dk Evelyne Lukonge, ambaye ni Mtafiti Kiongozi wa Chuo cha Utafiti cha Kilimo cha Ukiliguru kilichoko mkoani Mwanza.
Msomi huyu nilikutana naye wakati wa uzinduzi wa ripoti ya hali ya biashara ya mazao ya kibayoteki ya mwaka 2015, ambayo uzinduzi wake ulifanywa katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichoko Morogoro.
Baada ya uzinduzi ule, ambao ulifanywa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Dk Florens Turuka, nilifanya mazungumzo na mwanamama huyo na swali la kwanza kwake, lilihusu kilio cha mbegu feki za pamba, zao ambalo ni maarufu katika Kanda ya Ziwa.
Kwa nini wakulima wanagawiwa mbegu feki wakati tuna wasomi kama yeye kwenye vyuo vya utafiti? Nilimuuliza swali hilo la mbegu feki mtaalamu huyu, kwa kuwa kilio kikubwa kwa wakulima wa zao la pamba walioko Kanda ya Ziwa kwa miaka ya hivi karibuni, imekuwa ni mbegu feki zisizoota.

Image result for picha za zao la pamba
Kuna kampuni nyingi ambazo zinasambaza mbegu kwa wakulima na mbegu hizo zimewapa hasara wakulima kwa kuwa hazioti. Kama mdau wa zao la pamba na kwa kuwa nilisomeshwa kwa fedha za zao la pamba, jambo hili limekuwa linaniumiza.
Katika majibu yake, mtaalamu huyu aliniambia kwamba mfumo wa mbegu za pamba una changamoto nyingi, kwani watafiti wanaweka viwango na kuwaachia kampuni zinazozalisha mbegu na kuwasambazia wakulima kufanya uzalishaji.
Mfumo huu umewapa fursa wazalishaji wa mbegu kuzalisha mbegu, ambayo haina ubora na hivyo kutoota pale inapopandwa. Kuna baadhi ya wasambazaji wa mbegu za pamba, wamekuwa wanazalisha mbegu katika maeneo yaliyobainika kuwa na ugonjwa wa mnyauko fusari (fusarium wilt disease), ambao nao umekuwa chanzo cha mbegu kutoota.
Wakati yote haya yanafanyika kuna Wizara ya Kilimo, kuna Bodi ya Pamba na taasisi inayohusika na udhibiti wa ubora wa mbegu (TOSCI), wote hawa wanahusika kuhakikisha mkulima anapatiwa mbegu bora. Pamoja na uwepo wao, lakini mkulima wa Pamba imeendelea kuumizwa na wafanyabiashara.
Kitendo cha mbegu kutoota ni hasara kwa mkulima kwa sababu kwanza mkulima ametumia fedha kununua mbegu hizo, hivyo kwake inakuwa ni hasara kubwa. Lakini kitendo cha kutopata mazao ni hasara kubwa kwa mkulima huyu.
Baadhi ya kampuni pia kwa makusudi zimekuwa zinasambaza mbegu zilizooza kwa kwa wakulima. Hilo lilitokea mwaka jana huko wilayani Bunda mkoani Mara, ambako kuna kampuni zilisambaza tani 40 za mbegu za pamba ambazo zilikuwa zimeoza na matokeo yake hazikuota na kuwapa hasara kubwa wakulima.
Serikali yenyewe pia imekuwa inapata hasara kwa kukosa kodi, ambayo ingetokana na zao la Pamba. Wakati wakulima wanaendelea kutaabika, viongozi wa kisiasa wa wizara, mikoa, bodi ya pamba na TOSCI wamebaki kutoa matamko tu ya kuwaonya wasambazaji wa mbegu feki kuacha mara moja, la sivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Pamoja na matamko hayo, hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya wasambazaji hao matapeli. Binafsi nashauri kwamba kuna mfumo mbovu wa kusambaza mbegu za pamba kwa wakulima, na kwa kuwa kampuni zinazofanya biashara hii, zimekuwa zikipata faida kubwa na kuwaacha wakulima wanaogelea kwenye umaskini, ni vyema kampuni ikibainika kusambaza mbegu feki, ifutiwe usajili mara moja na wahusika wafikishwe mahakamani.
Serikali ndiyo msimamizi mkuu na mwenye kutoa leseni kwa kampuni zinazosambaza mbegu nchini, Bodi ya Pamba ni wataalamu katika kuishauri serikali namna ya kuzalisha pamba kwa tija, TOSCi wanadhibiti ubora wa mbegu; hivyo mamlaka tatu hizi, zinatakiwa kuchukua hatua kwa kuzifutia leseni kampuni zote, ambazo zitasambaza mbegu feki au mbegu zilizooza kwa wakulima wa pamba.

Image result for picha za zao la pamba

Previous
Next Post »