Propellerads

Vijana na Fursa za Viwanda.....



Image result for picha za viwanda

VIJANA ni nguvu kazi ya taifa inayopaswa kuandaliwa ipasavyo, ili itoe mchango unaotakiwa kukuza uchumi wa nchi na hatimaye kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Ni dhahiri kuwa taifa lililo na vijana walioandaliwa vizuri katika uzalishaji, iwe kupitia shambani (Kilimo) au kwa kuwajibika ofisini, kwa mtindo wa utendaji kazi wenye ufanisi na unaoleta tija, lina nafasi nzuri ya kupata maendeleo, hasa kama vijana hao watatumiwa kwenye maeneo waliyo na ujuzi.
Imekuwa ikielezwa na inaendelea kuelezwa na wataalamu wa masuala ya maendeleo katika maeneo mbalimbali duniani kuwa, vijana ndio kundi kubwa la watu wenye nguvu kwenye mataifa duniani. Halihitaji kuachwa lipotee.
Kwa kufahamu ukweli huo, mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea duniani, likiwemo la Tanzania, yanapiga vita mbinu na hila zinazoonekana kuwa kikwazo cha maendeleo ya vijana, kwa sababu zinachangia kwa kiasi kikubwa kuwadhoofisha.
Dawa za kulevya ni janga linalotajwa karibu kila kona ya dunia kuwa changamoto kubwa inayotakiwa kutafutiwa ufumbuzi, kwa kuwa zinaharibu akili za vijana, kudhoofisha miili yao na kuwageuza vioja kutokana na matukio mabaya wanayoshiriki kuyatenda ili angalau kujipatia kipato.
Wanaotumia dawa za kulevya huishia kuwa ‘mateja’ wasioweza kushiriki shughuli za maendeleo mfano uzalishaji shambani au ofisini, hivyo kuwa tegemezi kwa taifa.
Vijana wengi wanaotumia dawa hizo wamekuwa kero kwa jamii inayowazunguka, kutokana na kujiingiza katika matukio ya uhalifu, ikiwemo ujambazi, ubakaji, wizi na uporaji wa mifukoni, uuaji na matukio ya uharamia na ujangili yanayohusu uhujumu uchumi.

Image result for picha za viwanda
Pamoja na mapambano dhidi ya wanaotaka kuangamiza nguvu kazi hii, Serikali imekuwa mstari wa mbele kusisitiza mafunzo ya uzalishaji kwa vijana huku ikitoa fedha kufadhili mafunzo mbalimbali, ili kuwaandaa vijana kushiriki uzalishaji.
Alhamisi iliyopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema Serikali imetenga Sh bil 15 kujengea kundi hilo uwezo kupitia mafunzo, ili lishiriki kama nguvu kazi katika uzalishaji pindi viwanda vitakapoanza. Alitoa kauli hiyo kwenye sherehe za utoaji tuzo ya mwajiri bora wa mwaka 2016, iliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na kufanyika Dar es Salaam siku hiyo.
Tunaamini kujielekeza kwa Serikali kuelimisha vijana hasa kwa kuangalia sekta za kipaumbele kutawafanya vijana wengi washiriki uzalishaji na kulifanya taifa linufaike. Jambo la msingi tunaloliona sisi ni vijana wenyewe kuchangamkia mafunzo hayo wakati wowote yanapotolewa na kuacha kujiweka nyuma kwa kujipuuza, kurubuniwa au kufikiria kuwa yana wenyewe.


Ni vema vijana wakafahamu kuwa wanaostahili mafunzo hayo ni wao na wakiyapata na kuyatumia ipasavyo katika uzalishaji, watakaonufaika ni wao na taifa pia. Hongera Serikali kwa kuwaandaa vijana kujiajiri na kuajiriwa na kwa kuhakikisha sekta binafsi nayo inapata nafasi ya kukua na kutoa ajira kwa vijana.
Previous
Next Post »