MFUMUKO wa bei wa taifa kwa mwezi Novemba umeongezeka hadi kufikia asilimia 4.8 kutoka asilimia 4.5 iliyokuwa mwezi Oktoba, mwaka huu.
Kuongezeka kwa mfumuko huo, kunatokana na kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula, ambayo imeongezeka hadi kufikia asilimia 6.2 kutoka asilimia 6.0 ilivyokuwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu, Ephraim Kwesigabo alisema katika takwimu za kipindi kinachoishia mwaka huu, makundi ya bidhaa mbalimbali yamepanda kwa kiasi kidogo.
Kwesigabo alisema kuongezeka kwa mfumuko wa bei kunamaanisha kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba imeongezeka ikilinganishwa na kasi ya upandaji ilivyokuwa kwa mwaka ulioshia Oktoba mwaka huu.
“Kuna vitu vingi vimesababisha kupanda kwa mfumuko wa bei ni bidhaa za vyakula…mahindi yamepanda kwa asilimia 16.6, kitoweo kama samaki vyote vimepanda kama kwa asilimia 23.7,” alisema mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa kwa upande wa nishati, matumizi makubwa ni kwa mkaa ambao umepanda kwa asilimia 22.1.
Vingine vimepanda kidogo kama vinywaji, tumbaku na gharama za afya. Kwesigabo alisema mfumuko wa bei kwa bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula kwa kipimo cha mwaka wa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani kwa mwezi Novemba mwaka huu, umeongezeka hadi asilimia 6.4 kutoka asilimia 6.0 kwa mwezi Oktoba.
“Hizi ni baadhi tu ya bidhaa ambazo zimeonesha kupanda kati ya mwezi Oktoba na Novemba bila kusahau dizeli nayo imepanda kidogo, tunaposema kupanda hatumaanishi Dar es Salaam peke yake bali nchi nzima,” alieleza.
Aidha, fahirisi za bei zimeongezeka hadi 104.32 mwezi Novemba kutoka 99.54 kwa kipindi kama hicho mwaka jana. Fahirisi za bei kwa bidhaa zisizo za vyakula limeongezeka hadi asilimia 3.8 mwezi Novemba kutoka asilimia 2.9 kwa Oktoba mwaka huu.
Ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika Mashariki, Kenya mfumuko umeongezeka hadi asilimia 6.68 kutoka asilimia 6.42 mwezi Oktoba, mwaka huu wakati Uganda nako mfumuko wa bei wa mwezi Novemba umefikia asilimia 4.6 kutoka 4.1.
ConversionConversion EmoticonEmoticon