HAJAWAHI kukosea, pamoja na ukongwe wake kwenye muziki wa bongo flavor lakini anawazidi wakongwe wenzie wengi. Msanii huyu hakuna wakati ametoa wimbo ukashindwa kukamata na kupendwa na wadau wa muziki, huyo ndiyo Khamisi Mwinjuma, maarufu mwana Fa.
Msanii huyu alianza kuvuma kwenye muziki tangu miaka 2000, akiwa na kundi wa East Coast chini ya usimamizi wa Gwamaka Kaihula ‘King Crayz GK’, Ambwene Yessaya ‘AY’, O ten na wengine wengi. Wimbo ambao ulilitambulisha kundi hili miaka hiyo ya 2000 ulikuwa ama zangu ama zao, waliouimba kwa kumshirikisha mkongwe mwingine kwenye fani, Lady Jaydee ‘Jide’.
Mwana Fa ametamba na nyimbo nyingi, ukiwemo mabinti ambao pia ulijizolea umaarufu kwa mabinti. “Mi na mabinti dam dam kweli.. kwelii,” anaimba mwana Fa enzi hizo katika wimbo huo mabinti.
“Yaani shwari hamna sharii, me na mabinti dam dam,” anaimba mwana Fa kwenye wimbo huo ambao ni miongoni mwa nyimbo zilizomtambulisha kwenye ‘game’.
Kwenye wimbo huu, mwana Fa alizungumzia zaidi uhusiano wake na mabinti kwamba ni rafiki zake wa karibu. Lakini Mwana Fa ambaye mara nyingine pia hupenda kujiita Binamu, alitoka na wimbo wa Unanitega aliomshirikisha msanii kutoka Chamber Squad Noorah. Hapo alizungumzia zaidi jinsi binti anavyovaa nguo akiacha maungo yake wazi, hapo ndipo anapomuuliza unanitega?
Mwana Fa pia alishatamba na wimbo wa Alikufa kwa Ngoma aliomshirikisha Jide, Hawajui alioimba na Jide pia. Ameendelea kuwa msanii mkongwe mwenye vionjo vya kipekee ambaye anapotoa wimbo hakuna atakayethubutu kutoupenda na kujihoji nini haswa msanii huyu alichofikiria na kuamua kuimba wimbo husika.
Kuna nyimbo kadhaa huwa zinazusha mjadala kwenye jamii ukiwemo bado nipo nipo sana ambao anaeleezea sababu za kuchelewa kuoa.
Baada ya miaka mingi kupita tangu atoe wimbo huo, msanii huyo alifunga ndoa katikati ya mwaka huu.
“Mwana Fa utaoa lini, bado nipo nipo sana,” ndivyo anavyojibu swali analoulizwa na mmoja wa wasanii alioimba nao kwenye wimbo huo.
“Aliyelala na bi harusi siku moja kabla ya harusi na wala sio bwana harusi bado mnanishauri harusi?” Anahoji mwana Fa kwenye wimbo huo. “Eri nizibe masikio, wengine nifumbe macho nisione wakati naibiwa?
So mpaka miaka mingi ijayo ndio mniulize nitaoa lini,” anaendelea kumwaga mistari mwana Fa kwenye wimbo huo uliozua mjadala kwenye jamii na vijana wengi kuutumia kama sababu ya wao kutokuoa. Mwaka jana alikuja na kibao cha Asanteni kwa kuja, ambao kama ilivyo kwa wasanii wengine kwenye wimbo huu alilenga kuburudisha zaidi.
Lakini kama ilivyo kawaida ya mwana Fa, wimbo huo nao ulishika chati kwa kupendwa na mashabiki mbalimbali wa muziki. Wiki mbili zilizopita kaibua kitu kingine kilichozua mjadala tena kama ilivyo kawaida yake mkongwe huyo. Dume Suruali ndio habari ya mjini kwa sasa, ukionekana kupokewa zaidi na wanaume kwani sasa wanaona kama wamepata mtetezi.
“We ni dume suruali kaa mbali nami mbali nami kama dume suruali kaa mbali nami huendani nami,” analalamika Vanesa Mdee aliyeshirikishwa kwenye wimbo huo, akimtaka Mwana Fa kuwa mbali naye maana ni dume suruali haendani naye.
“Hudat hudat ni salam na ufahamu kama unauza mapenzi sio kwa binamu hakuna haja ya kusubiri hii ni hukumu hakuna kitu utapata, utangoja kama askari wa zamu, dume suruali, dume kapura shauri zako ili mradi nisipate hasara,” anajibu Mwana Fa shutuma hizo za kuambiwa dume suruali.
Hii kauli ya dume suruali hutumika sana kwa wanawake wakiwaita wanaume wasiowapa fedha kwamba ni wanaume suruali. Katika mahojiano maalumu na Mwana Fa, anaeleza sababu za kuamua kuimba wimbo huo.
“Lengo ni kuwazungumzia wanawake ambao wanaowaona wanaume ni ATM, shimo la madini yaani kila anachokifuata kwa mwanaume ni masuala ya kiuchumi, wimbo ndio ulikuwa na maana hiyo, vitu vingine vyote vimewekwa kurahisisha tu kisanii…
“Kisanii unajua unaweza kuwa unatengeneza wimbo unaohusiana na masuala ya ukimwi lakini ukasema alikufa kwa ngoma, watu wapate shauku kusikiliza unataka kusema nini… “Lakini wimbo umelenga eidha wanawake wamezidisha hiyo tabia na wanaume wawe wakali kidogo,” anasema.
“Usione utani mi sihongo hata kwa ishara utaniambia nini mpaka unigeuze fala, kwanza nasikia hongo zinaleta mikosi sentano yangu hugusi hata ukiongea kidosi… yabaki mapenzi tusileteane ujambazi hata upige sarakasi utachonga viazi…” anazidi kulalama mwana Fa kwenye wimbo huo na hapo ndipo anapofafanua kwamba wanawake wamezidisha tabia ya kuwageuza wanaume vitegauchumi.
“Bahili kama nini,” anajibu Vanesa kwa hasira. Lakini mkongwe huyo anajibu: “Ndivyo mnavyosema, na ukiomba kesho hunisikii tena kwani unauza nini dada hunitakii mema…
Nihonge nanunua nini kwa nini yani kuna kipi nisichokijua ina Tv ndani, usiniulize nitakupa nini dada piga moyo konde, viuno vingi kama mwali wa kimakonde, usipende hela kama mfuko au fanya utakavyo upate zako, vishawishi vingi binti sema na moyo wako na ujifunze pesa zinauza utu wako, tajiri mtata kama salah, zipo ila sitoi sio bahili mi ni balaa, unapenda hela zangu na mimi nazipenda pia kila mtu abaki na zake, bye baby tutaongea,”
Anarusha madongo mwana Fa na kumuacha hoi Vanesa anayemalizia “Mwanaume wa hivyo wa nini sasa”.
Ukisikiliza wimbo huo unagundua pia mwana Fa anawatahadharisha wanake wanaopenda wanaume kwa sababu ya fedha kwamba wanauza utu wao. Siri ya mafanikio yake ni nini kulinganisha na wakongwe wenzie ambao wameshapotea muda mrefu kwenye game?.
“Tatizo vitu vingi naweza kusema, wakati mwingine unaweza kuwa na bahati, wakati mwingine malengo unayojiwekea huwezi kusema ni makosa yao, pengine waliwaza vibaya hakuna mtu anapenda kupotea kwenye fani, labda wengine tulikuwa na bahati kwamba mipango tuliyojiwekea na ndiyo ilivyokuwa,” anasema.
Mwana Fa anazungumzia wasanii wa sasa wa muziki wa kizazi kipya na hapa anazungumzia bifu la marafiki Nasib Abdul ‘Diamond’ na Omari Nyembo ‘Ommy Dimpoz’. Akisema bifu lao linachangamsha sekta hiyo na kusisitiza muhimu ni kudhibiti wasizuriane.
“Unajua hakuna kitu kisichokuwa na ushindani, mfano wewe upo Daily News lazima mtakuwa na washindani wenu, mnachotakiwa kufanya ninyi waandishi ni kujizuia msizuriane…
“Inachangamsha muziki unapata wa kuwazungumzia, kukiwa na ushindani wa hapa na pale sifikiri kama ni kitu unachoweza kukizuia, game ikiwa rafiki sana nayo inakuwa haiwezi kuburudisha, haiwezekani mashabiki wawe wote wa wanamuziki wote hakuna kitu kama hicho,” anasema.
Mwana Fa anaahidi bado ana mambo mengi ya kufanya katika kuendeleza muziki lakini pia kuendeleza familia yake pamoja na masuala ya biashara”.
ConversionConversion EmoticonEmoticon