MFANYABIASHARA maarufu nchini, Mohammed `Mo’ Dewji ameendelea kung’ara kimataifa, baada ya juzi kufanikiwa kutwaa tuzo ya `Mjasiriamali wa Mwaka-Biashara barani Afrika’ jijini Paris, Ufaransa.
Licha ya kushukuru kwa tuzo hiyo, amepigia debe uwekezaji Tanzania, akiitaka Ufaransa kugeukia uwekezaji katika ardhi ya Tanzania ambayo Rais wake, Dk John Magufuli amekusudia kuipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.
Tuzo hiyo iliyoandaliwa kwa mara ya kwanza na taasisi ya Movement of the Enterprises of France (MEDEF) kwa kushirikiana na taasisi nyingine ya Choiseul Institute, imekwenda kwa Dewji kutokana na mafanikio yake makubwa kibiashara barani Afrika, kiasi cha kuwa mfano wa kuigwa.
Medef, taasisi iliyoanzishwa mwaka 1988, ndiye mwajiri mkubwa Ufaransa, ikiwa na makampuni makubwa kama Total, BNP Paribas, AXA Group, Michelin na L’Oreal. Akizungumza katika tuzo hizo, Dewji alishukuru na kuelezea dhamira yake ya kutaka kuona sekta binafsi inachangia kupaisha uchumi na maendeleo ya bara la Afrika.
“Mipango endelevu ya muda mrefu ndiyo itakayoifanya sekta binafsi kuipaisha Afrika. Na ili hayo yatimie, kampuni binafsi zinapaswa kuwashirikisha wasio na kipato kuwa wazalishaji, wasambazaji, waajiri na wanunuzi, kama inavyofanya MeTL Group nchini Tanzania,” alisema Dewji (41).
Aidha, alitumia fursa hiyo kuishauri Ufaransa kugeukia uwekezaji katika nchi zisizozungumza Kifaransa zikiwamo za Afrika Mashariki akisema ni mahali pazuri pa uwekezaji kwa kuwa kuna utulivu wa kisiasa na soko la uhakika kutokana na wingi wa raia wake.
Aliongeza kuwa, hilo linajidhihirisha kwa jinsi Rais Magufuli alivyogeuka gumzo kutokana na kasi yake ya utendaji kazi, ikiwa ni pamoja na kupiga vita vitendo vya rushwa, uzembe na mambo mengine yanayorudisha nyuma maendeleo ya taifa.
“Rais wa Tanzania ni mfano kwa sasa Afrika na duniani. Akili yake ipo katika maendeleo na uwajibikaji. Watu wameanza kumwelewa na Watanzania wameanza kubadili staili za maisha, kila mmoja akiwaza kuchapa kazi ili kujiletea maendeleo yake na taifa kwa ujumla,” alisema Dewji ambaye pia ni Rais na Mtendaji Mkuu wa MeTL Group aliyeitoa tuzo yake kwa vijana wa Afrika anaoamini wana nafasi ya kufanya mapinduzi ya kimaendeleo barani humo.
Aliwataka vijana, bila kujali wako katika mazingira magumu kiasi gani, wasikate tamaa, akisisitiza wana nafasi kubwa ya kufanya mapinduzi ya kweli ya kimaendeleo kwa bara la Afrika.
Tuzo hiyo imezidi kumpaisha Dewji kimataifa, kwani katika miaka ya hivi karibuni ametwaa tuzo kadhaa, ikiwamo ya ‘Mtu Maarufu Afrika kwa mwaka 2015’ kwa mujibu wa jarida maarufu la uchumi na biashara duniani, Forbes la Marekani.
Amewahi kutwaa pia tuzo ya Mfanyabiashara Bora wa Afrika akimpiku bilionea namba moja Afrika, Aliko Dangote wa Nigeria. Pia ndiye kijana tajiri zaidi Afrika. Kampuni yake yenye makampuni tanzu 31 nchini, ndiyo inayoongoza kwa kutoa ajira Tanzania, kwani imeajiri watu 26,000 lakini akilenga kufikisha ajira 100,000.
ConversionConversion EmoticonEmoticon