MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,Dar es Salaam imeamuru mwili wa Ernest Materego aliyefariki dunia Dar es Salaam na kusafirishwa hadi Bunda mkoani Mara, urejeshwe Dar es Salaam na kuzikwa na watoto na mke wa marehemu.
Hatua hiyo inatokana na mgogoro wa familia kuhusu maziko ya Materego aliyeaga dunia Novemba 19, mwaka huu. Watoto wakitaka baba yao azikwe Dar es Salaam wakati ndugu wengine walishasafirisha mwili wa marehemu hadi Bunda.
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Thomas Simba alitoa uamuzi huo jana ikiwa ni siku 16 tangu Materengo afariki dunia.
Kesi hiyo ilifunguliwa na watoto wa marehemu ambao ni Joyce, Edwin, Ritha, Irene Materego pamoja na mama yao, Dinah Willige (65) dhidi ya mdogo wa marehemu, Gonche Materego.
Akisoma uamuzi huo jana, Hakimu Simba alisema mwili huo uliokuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Bunda, unatakiwa kuchukuliwa na watoto na mke wa marehemu, na kuurudisha Dar es Salaam kwa ajili ya kumzika mpendwa wao.
Aidha, aliutaka upande wa wadaiwa kuwapa watoto hao kibali cha kumzika baba yao na wakati wa mazishi kuwa na usalama, pia alisema kila upande utabeba gharama zake, ikiwemo za kusafirisha mwili kutoka Bunda.
Hakimu Simba alisema ametoa uamuzi huo kwa kuwa baada ya kupitia ushahidi, ameona hakukuwa na makubaliano kati ya wanafamilia, watoto pamoja na mke wa marehemu kuhusu mazishi.
Alisema kwa mujibu wa ushahidi kabla mwili wa marehemu haujasafirishwa kwenda Bunda kulikuwa na makubaliano ya kumsuburi mke wa marehemu aliyekuwa Nairobi pamoja na mtoto wake aliyekuwa Marekani lakini hawakufanya hivyo.
Aidha, alisema ushahidi uliotolewa na mke na watoto wake umeeleza kuwa, wakati wa uhai wake Materego alitaka azikwe Dar es Salaam.
Alisema ingawa Gonche na Mwajuma Hassan (anayedaiwa kuwa mke mdogo wa marehemu) walieleza kuwa, Materego alitaka azikwe Bunda lakini anaamini watoto na mke aliyefunga naye ndoa mwaka 1970 na walikuwa wakiishi pamoja, ndiyo wameeleza ukweli.
Katika ushahidi wake, mke wa marehemu Materego, Dinah Willige alidai kuwa alifunga ndoa na mume wake mwaka 1970, wakafanikiwa kupata watoto wanne na walikubaliana mmoja wao akifa mke au mume aulizwe azikwe wapi.
Aliendelea kudai kuwa yeye alikuwa anaishi Nairobi, Kenya kwa sababu ya kazi na ndoa yao ilikuwa na matatizo tangu mwaka 2010, lakini mume wake alipofariki Gonche alimpigia simu na kumtaarifu kuwa wamehifadhi mwili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Alidai baada ya kupata taarifa hizo alimwambia wasizike wamsubiri yeye pamoja na mtoto wake anayeishi Marekani ili wakubaliane, lakini baadaye alipigiwa simu na kuambiwa wanasafirisha mwili kwenda Bunda “nilikataa kwa sababu mume wangu aliniambia akifa azikwe Dar es Salaam.”
Aliongeza kuwa alifika Dar es Salaam, Novemba 26, mwaka huu na kukuta mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda Bunda.
Gonche alidai ndoa ya Dinna na kaka yake ilikuwa imevunjika tangu mwaka 2009 na kuwasilisha hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Mwanzo ya Ukonga Agosti 25, 2009 pamoja na hati ya talaka, lakini Dinna alidai hajui kuhusu jambo hilo, na kudai kulikuwa na matatizo kwenye ndoa yao, lakini hawakuachana na mume wake.
Alidai kuwa kaka yake alioa mke mwingine, Mwajuma Hassan (39) na wana mtoto mmoja, Waitara aliyezaliwa 2008 na katika uhai wake Materego alimwambia yeye, Mwajuma na mama yake kuwa akifa akazikwe Bunda. Mwajuma alidai yeye ni mke wa Materego walifunga ndoa ya kimila mwaka 2013, lakini hana cheti cha ndoa.
Source; Habari leo
ConversionConversion EmoticonEmoticon