WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, ameomba ndege za serikali (Bombardier) zianzishe safari ya kati ya Dar es Salaam na Iringa kwa Dola za Marekani 150 (sawa na zaidi ya Sh 300,000) ili kukuza utalii katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yenye vivutio lukuki.
Pamoja na ushauri huo, amemkumbusha mmiliki wa Hoteli ya Peacock ya Dar es Salaam, Joseph Mfugale, kumalizia ujenzi wa hoteli ya nyota tano mjini Iringa ili kuboresha na kuongeza huduma za hoteli ambayo ni moja ya changamoto zinazokwamisha ukuaji wa sekta hiyo mkoani Iringa.
Ujenzi wa hoteli hiyo inayojengwa karibu na Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (RUCU) ulianza kwa kasi kubwa mwanzoni mwa mwaka 2008, lakini ukasimama miaka miwili baadaye.
Akizindua maonesho ya Karibu Kusini na Siku ya Utalii Duniani iliyoanza kufanyika kitaifa mjini Iringa juzi, Profesa Maghembe alisema huduma ya usafiri wa anga na ukosefu wa hoteli nzuri katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ni baadhi ya mambo yanayozorotesha ukuaji wa sekta hiyo.
“Tunataka watalii kutoka nje waje kwa wingi Kusini, lakini wanakwazwa na gharama kubwa za usafiri wa ndege, miundombinu mibovu ya barabara na huduma mbovu za hoteli,” alisema.
Aliahidi kuishauri Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kuanzisha safari za gharama nafuu kati ya Dar es Salaam, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe, Ruvuma na Katavi ili kuwahamasisha watalii kutembelea vivutio katika mikoa hiyo.
Pia alisema halmashauri za mikoa hiyo zitenge maeneo kwa ajili ya ujenzi wa hoteli zenye hadhi ya nyota nne na tano ili kuvutia watalii hasa wa nje huku akiwahakikishia wadau kwamba serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu katika vivutio vya mikoa hiyo.
Kabla ya uzinduzi wa maonesho hayo, Profesa Maghembe alitembelea mabanda ya wadau mbalimbali yanayotangaza shughuli mbalimbali zinazohusiana na utalii nchini.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema mkoa kwa kushirikiana na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, umeanzisha maonesho ya Karibu Kusini yatakayokuwa yakifanyika kila mwaka ukiwa ni mkakati wao wa kuhamasisha utalii wa vivutio vya kusini mwa Tanzania.
Masenza alisema uamuzi huo umefanywa baada ya mkoa huo, mwaka 2009 kuteuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa kitovu cha utalii kwa mikoa ya Ruvuma, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa inayounda kanda hiyo. Akifafanua kuhusu vivutio vilivyopo katika mikoa hiyo, Masenza alisema vipo vya kihistoria, kiutamaduni, na kiikolojia.
IMEANDIKWA NA FRANK LEONARD, IRINGA
ConversionConversion EmoticonEmoticon