Propellerads

Tambwe abaki njia panda


Image result for picha za tambwe

YANGA huenda ikampoteza mshambuliaji wake, Amis Tambwe ambaye mkataba wake unaelekea ukingoni, kwani hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote waliyofanya naye.
Tambwe amebakiza miezi mitano tu katika mkataba wake wa sasa unaotarajia kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Huenda Yanga wakawa hawana mpango tena na wanataka kuachana naye mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita na msimu wa mwaka juzi.
Akiwa Yanga msimu uliopita alifunga mabao 21 wakati akiwa na Simba msimu wake wa kwanza katika Ligi Kuu Tanzania Bara, alifunga mabao 19.
Kutokana na sheria za soka mchezaji anapobakiza mkataba wa miezi sita anaweza kufanya mazungumzo na timu nyingine au hata kusaini mkataba wa awali, endapo timu yake anayoichezea haitamuongezea mkataba.
Akizungumza na gazeti hili jana, Tambwe alisema kwa sasa hajapata ofa yoyote, lakini ikitokea baada ya mkataba wake na Yanga kuisha yuko tayari.
“Bado nina mkataba na Yanga, sijafanya mazungumzo yoyote ya kuongezewa mpaka sasa, siwezi kusema nitaenda wapi, nasubiri ukiisha tu, nitaweka wazi,”alisema.
Mchezaji huyo wa zamani wa Simba alisema ni mapema mno kuamua kama ataondoka Jangwani, akiamini ana nafasi ya kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema wanamhitaji mchezaji huyo kwa kuwa ana ubora usiokwisha, na kwamba watafanya naye mazungumzo kumuongezea mkataba mpya.
Tambwe amefunga mabao manane katika mzunguko wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, akishika nafasi ya pili nyuma ya Shiza Kichuya anayeongoza akiwa ametupia tisa.
Wakati huo huo, beki Mtogo wa Yanga, Vincent Bossou alitarajia kuwasili jana na leo kujiunga na wenzake katika mazoezi ya timu hiyo tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotazamiwa kuanza Desemba 17.
Bossou akiwasili atafanya idadi ya wachezaji walioripoti mazoezini Yanga kufika 24 tangu kocha mpya, Mzambia George Lwandamina aanze kuifundisha timu hiyo.
Previous
Next Post »