MKUU wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel amesema kamwe hatamvumilia kiongozi wa kisiasa atakayebainika kufanya uovu huku akitegemea kulindwa na chama anachokitumikia, akisema yeyote atakayebainika kuhusika atashughulikiwa kisheria.
Ametoa rai hiyo jana alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Kerenge Kibaoni wilayani hapa kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo.
Alisema katika uchunguzi alioufanya tangu alipowasili wilayani Korogwe mpaka sasa amebaini shida nyingi za wananchi zimesababishwa na baadhi ya viongozi ambao wanalalamikiwa na wananchi.
“Viongozi wa aina hii wamekuwa chanzo cha migogoro mbalimbali ikiwemo ile ya ardhi pamoja na kero za wakulima na wafugaji, Kutokana na hali hiyo napenda kuweka bayana kwamba nitawashughulikia viongozi wote hasa wa kisiasa watakaobainika kuwahujumu wananchi huku wakitegemea kujificha kwenye vyama vyao,” alisema.
Aidha, mkuu huyo aliwahimiza viongozi hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa misingi ya haki ili kupunguza malalamiko na kuwawezesha kujenga imani na serikali yao.
Awali katika mkutano huo wa hadhara wananchi walimweleza DC huyo kwamba wanakabiliwa na upungufu wa wataalamu kwenye zahanati yao, ukosefu wa maji safi na salama hivyo kulazimika kutumia maji machafu.
ConversionConversion EmoticonEmoticon