KAMA falsafa yake inavyojieleza ya ‘Hapa Kazi Tu’, Rais John Magufuli amepeleka falsafa hiyo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kufumua muundo wake baada ya kutangaza kupunguza idadi ya wajumbe wa vikao na idadi ya vikao katika ngazi mbalimbali ili viongozi watumie muda mwingi kufanya kazi za chama.
CCM imesema uamuzi huo, una lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji wa chama na kuongeza muda wa viongozi kufanya kazi za chama kwa umma, badala ya kutumia muda mwingi vikaoni. Sanjari na kufuta baadhi ya vyeo, pia imetangaza uhakiki wa wanachama wake kote nchini na kuanzisha mfumo wa kadi za kielektroniki na kuachana na kadi za sasa, zikiwamo za jumuiya yake ambazo zinafutwa rasmi.
Mabadiliko hayo makubwa ambayo baadhi yanahusisha Kanuni na Miongozo, yataanza mara moja na yale yanayohusisha Katiba ya CCM yatapata idhini ya Mkutano Mkuu utakaoitishwa Februari mwakani, na yamefanywa jana na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) katika kikao chake kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Hicho kilikuwa kikao cha kwanza cha NEC chini ya Mwenyekiti mpya, Rais John Magufuli aliyeteuliwa Julai mwaka huu, akirithi mikoba ya Dk Jakaya Kikwete ambaye jana alimsifu kwa kumuongoza vizuri na kwa hiari yake, kuachia uenyekiti wakati Katiba bado ilikuwa ikimruhusu, akieleza kuwa huo ndio utofauti wa CCM na vyama vingine.
Aliposhika hatamu za CCM mjini Dodoma, katika hotuba yake Dk Magufuli alieleza azma yake ya kuijenga CCM mpya, ikiwamo kuondokana na vyeo visivyokuwa na tija na pia kupunguza idadi ya wajumbe wakiwamo wa NEC.
Jana asubuhi akifungua kikao hicho kilichofanyika kwa mara ya kwanza Ikulu, alirejea azma yake hiyo na kuwataka wajumbe waunge mkono mapendekezo hayo ambayo yalikwishapata baraka za Kamati Kuu iliyokutana Jumapili. Dk Magufuli alisema mabadi liko na mageuzi hayo ni muhimu na yanapaswa kuwalenga wanachama walio chini.
“Tumekuja kwa ajili ya kufanya kazi. Mimi nipo pamoja nanyi, yaliyopita si ndwele, tugange yajayo ili kutengeneza chama chetu. Lakini si kwamba yaliyopita tumeyasahau, tuendelea kukijenga chama chetu,” alisema Dk Magufuli na kuongeza: “Mabadiliko na mageuzi haya ni muhimu sana hasa wakati huu, sisi katika Kamati Kuu tumeyapitia na kuyachambua, tumefanya hivyo kwa ajili ya chama chetu.”
Kwa mujibu wa Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnaye ambaye sasa amepatikana mrithi wake, aliwaeleza waandishi wa habari baada ya kikao hicho kuwa uamuzi huo umefanywa ili kuwa na vikao vyenye tija. Katika fyekafyeka hiyo, wajumbe wa NEC wamepunguzwa kutoka 388 hadi 158, wajumbe wa Kamati Kuu kutoka 34 hadi 24, wajumbe wa Kamati za Siasa za Mikoa wamepunguzwa watatu wakati wilayani wameondolewa wanne pamoja na kufutwa kwa vyeo vya Makatibu Wasaidizi wa Wilaya na Mikoa na wa Mchumi wa Wilaya na Mkoa.
Katika uamuzi huo, imeamuliwa kuwa sasa NEC itakuwa na wajumbe 158 kutoka wajumbe 388 wa sasa, na wajumbe hao wamepunguzwa kutoka miongoni mwao, wakiwamo wabunge ambao sasa watakuwa watano badala ya 10.
Kwa muundo huo mpya, wajumbe hao 158 watakuwa ni wenyeviti wa mikoa ambao ni Tanzania Bara, 26, Zanzibar sita, wajumbe wa NEC wa mikoa 26 Tanzania Bara na 24 (wanne kwa kila mkoa) Zanzibar, wajumbe wa NEC Taifa Bara 15 na Zanzibar 15, na nafasi saba za Mwenyekiti badala ya 10 za sasa.
Wengine ni wajumbe wa NEC wa jumuiya ambao ni UVCCM watano, UWT watano, Wazazi watano; wajumbe wa NEC kutoka bungeni watano, Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM mmoja, na wajumbe wa NEC kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) watatu watatu na Katibu wa Kamati ya BLW mmoja.
Nape aliwataja wajumbe wa NEC watakaoingia kwa nyadhifa zao ni Mwenyekiti wa CCM, Makamu Mwenyekiti Bara, Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Spika wa Bunge, Spika wa BLW, Mwenyekiti wa UWT, Mwenyekiti wa UVCCM, Mwenyekiti wa Wazazi pamoja na makatibu wao wakuu ambao pia ni watatu kufanya jumla ya wajumbe 158.
Aidha, kwa mujibu wa Nape, sasa vikao vya kawaida vya NEC vitafanyika kila baada ya miezi sita badala ya miezi minne kama ilivyo sasa isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalumu inapohitajika.
Kwa upande wa Kamati Kuu, panga nalo limepita kwa wajumbe kutoka 34 hadi 24 ambao watakaobaki ni Mwenyekiti, Makamu wake wawili, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu, Naibu wake wawili, Waziri Mkuu, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Spika wa Bunge, Spika wa Baraza La Wawawakilishi, wenyeviti watatu wa jumuiya, Katibu wa NEC Oganaizesheni, Itikadi na Uenezi, Uchumi na Fedha, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Wengine ni wajumbe watatu wa kuchaguliwa kutoka Tanzania Bara na wengine watatu kutoka Zanzibar, huku vikao hivyo sasa vimepunguzwa na vitakuwa vikifanyika kila baada ya miezi minne bada ya miwili ya sasa.
Kwa upande wa ngazi ya mkoa, walioondolewa katika Kamati ya Siasa ya Mkoa ni Katibu wa Uchumi na Fedha na wajumbe watatu wa kuchaguliwa, na vikao vyao vitakutana kila baada ya miezi mitatu na siyo kila mwezi kama ilivyo sasa.
Akizungumzia ngazi ya wilaya, Nape alisema wameondolewa Katibu wa Uchumi na Fedha, Katibu wa Kamati ya Madiwani na wajumbe wawili wa kuchaguliwa, na vikao vyao vuitakuwa vinakaa kila bada ya miezi mitatu badala ya kila mwezi.
Aidha, CCM imebadili muundo wake wa wilaya na kuanzia sasa muundo wa wilaya za Chama utaendana na muundo wa sasa wa serikali, kwa maana hakutakuwa tena na wilaya za chama kama sasa zilizo kwenye halmashauri mbili hata kama ziko wilaya moja kwa muundo wa Serikali. Pia kuanzia sasa idadi ya kuanzisha shina itakuwa wanachama 50 hadi 300, tawi iwe wanachama 301 hadi 1,000.
“Hata hivyo idadi hii izingatie eneo la kijiografia na wingi wa wanachama katika eneo hilo,” alifafanua Nape na kuongeza kuwa vikao vyao kwa ngazi hizo vitafanyika mara moja kila baada ya miezi mitatu.
Kuhusu nafasi moja, alifafanua kuwa mwanachama anatakiwa kuwa na nafasi moja tu ya uongozi kwa kazi ya muda wote kama ilivyoainishwa katika Kanuni za Uchaguzi Toleo la 2012 Kifgungu cha 22 na 23.
Alizitaja nafasi zilizoainishwa kuwa ni Mwenyekiti wa Tawi/ Kijiji/Mtaa, Mwenyekiti wa Kata/ Wadi, Mwenyekiti wa Jimbo, Wilaya na Mkoa, Makatibu wa Halmashauri Kuu kwa ngazi zote zinazohusika na Mbunge, Mwakilishi na Diwani.
Alisema NEC imeonya kuwa viongozi wa kuchaguliwa waepuke kuwa watendaji badala yake waongoze na kusimamia shughuli za chama kwa kuzingatia Katiba na Kanuni.
Akizungumzia vyeo ambavyo haviko katika Katiba ya CCM, alisema NEC imesema haviruhusiwi katika chama na jumuiya zake kama vile Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM, Makamanda wa Umoja wa Vijana, Walezi na Washauri katika ngazi zote.
Juu ya uhakiki wa wanachama, alisema, “Halmashauri Kuu imeona ipo haja ya kufanya uhakiki wa wanachama wa CCM na jumuiya zake ili kujua idadi sahihi ya wananchama wetu kwa wakati huu.” “Uhakiki huu uendane na kutoa kadi mpya za uanachama za kielektroniki ili kuwa na udhibiti wa usahihi wa wanachama na kuondoa wanachama hewa,” alisema Nape na kuongeza kuwa kadi za UWT, UVCCM na Wazazi zinafutwa na kubaki kadi moja ya CCM.
Alisema kwa sasa CCM ina wanachama zaidi ya milioni nane kwa hiyo uhakiki unafanyika ili kujiridhisha kama kweli inao wanachama hao, wamepungua au wamezidi ili kujitathimini hasa baada ya Uchaguzi Mkuu na pia kuwapo kwa madai kuwa wakati wa uchaguzi wa ndani baadhi ya wanachama huchomekwa kwa malengo ya kisiasa.
Aidha, alisema uendeshaji wa shughuli zote za jumuiya na mali zake sasa utakuwa chini ya usimamizi wa CCM wenyewe (Baraza la Wadhamini) zikiwamo ajira za watumishi katika jumuiya hizo zake tatu.
Katika moja ya maamuzi mengine makubwa, Nape alisema CCM inataka NEC imeona kwamba licha ya kutaka kubaki na bendera yenye rangi ya kijani na njano na alama ya jembe na nyundo, ipo haja ya rangi hizo kuzifanya ziwe na mwonekano wa kuvutia zaidi.
“Kwa hiyo, tutatafuta njia ya kuzifanya rangi hizo ziwe za kuvutia. Kama mtambuka mwaka jana wakati wa kampeni tulikuwa na fulana zenye rangi ya njano na kijani na nyeusi, tunataka kuzifanyia kazi na kuja na mwonekano wa kuvutia,” alieleza.
Kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar, NEC kwa mujibu wa Nape, imeagiza kuundwa kwa Kamati Maalumu ya kufanya tathimini ya kina kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar kwa ujumla na masuala yanayohusu Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Kwa wasaliti ndani ya chama hicho, wale ambao hawajachukuliwa hatua, wataendelea kushusha pumzi kwa muda baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Udhibiti na Nidhamu kutakiwa akamilishe kazi ya taarifa ya udhibiti wa wanachama waliokiuka mienendo ya kiuanachama klabla ya kuanza kwa Uchaguzi Mkuu wa chama Februari, 2017.
“Mikoa na Wilaya ambazo hazijaleta taarifa zao za kiudhibiti ziwe zimefikishwa taarifa zao kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Udhibiti na Nidhamu kabla ya tarehe 30/01/2017,” alieleza Nape akifafanua hatua hiyo, ambayo kwa mujibu wa Dk Magufuli, alipongeza wilaya na mikoa ambayo ilikwisha chukua hatua kwa wasaliti.
Alisisitiza kuwa kwa mambo ambayo ni masuala ya Miongozo na Kanuni yaanza mara moja, lakini kwa yale yanayohitaji mabadiliko ya Katiba ya CCM, Mkutano Mkuu utaandaliwa Februari mwakani na kutafakari na kupitisha mabadiliko hayo ya Katiba.
Kwa upande wake, alisema atakabidhi ofisi kesho Desemba 15, lakini akabainisha kuwa kazi yake ilikuwa katika kipindi kigumu katika miaka yake mitano ya kuwa Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi, akiwa na jukumu la kukisemea chama hicho kikongwe na tawala Tanzania.
ConversionConversion EmoticonEmoticon